Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Habakuki 3

Maombi ya Habakuki

Sala ya nabii Habakuki iliyoimbwa kwa shigionothi1.

Mwenyezi Mungu, nimezisikia sifa zako;

nami naogopa kwa matendo yako, Ee Mwenyezi Mungu.

Fufua kazi yako katika siku hizi zetu,

tangaza habari yako wakati huu wetu;

katika ghadhabu kumbuka rehema.

Mungu alitoka Temani,

yeye Aliye Mtakatifu kutoka Mlima Parani.

Utukufu wake ulifunika mbingu,

na sifa zake zikaifunika dunia.

Mng’ao wake ulikuwa kama jua linapochomoza;

miali ilimulika kutoka mkononi mwake,

ambako nguvu zake zilifichwa.

Tauni ilimtangulia;

maradhi ya kuambukiza yalifuata nyayo zake.

Alisimama, akaitikisa dunia;

alitazama, na kuyafanya mataifa yatetemeke.

Milima ya zamani iligeuka mavumbi

na vilima vilivyozeeka vikaanguka.

Njia zake ni za milele.

Niliona watu wa Kushani katika dhiki,

na makazi ya Midiani katika maumivu makali.

Ee Mwenyezi Mungu, uliikasirikia mito?

Je, ghadhabu yako ilikuwa dhidi ya vijito?

Je, ulighadhibikia bahari

ulipoendesha farasi wako

na magari yako ya vita ili ushinde?

Uliufunua upinde wako

na kuitisha mishale mingi.

Uliigawa dunia kwa mito;

milima ilikuona ikatetemeka.

Mafuriko ya maji yakapita huko;

vilindi vilinguruma

na kuinua mawimbi yake juu.

Jua na mwezi vilisimama kimya mbinguni

katika mng’ao wa mishale yako inayoruka,

na katika mng’ao wa mkuki wako umeremetao.

Kwa ghadhabu ulipitia kwenye dunia,

na katika hasira ulikanyaga mataifa.

Ulikuja kuwaokoa watu wako,

kumwokoa uliyempaka mafuta.

Ulimponda kiongozi wa nchi ya uovu,

ukamvua toka kichwani hadi wayo.

Kwa mkuki wake mwenyewe ulitoboa kichwa chake

wakati mashujaa wake walifurika nje kwa kishindo kututawanya,

wakifurahi kama walio karibu kutafuna

wale wanyonge waliokuwa mafichoni.

Ulikanyaga bahari kwa farasi wako,

ukisukasuka maji makuu.

Nilisikia na moyo wangu ukagonga kwa nguvu,

midomo yangu ikatetemeka kwa hofu niliposikia sauti;

uchakavu ukanyemelea mifupa yangu,

na miguu yangu ikatetemeka.

Hata hivyo nitasubiri kwa uvumilivu siku ya maafa

kuyajilia mataifa yaliyotuvamia.

Ingawa mtini hauchanui maua

na hakuna zabibu juu ya mizabibu,

ingawaje mzeituni hauzai,

na hata mashamba hayatoi chakula,

iwapo hakuna kondoo katika banda,

wala ng’ombe katika zizi,

hata hivyo nitashangilia katika Mwenyezi Mungu,

nitamfurahia Mungu Mwokozi wangu.

Bwana Mungu Mwenyezi ni nguvu yangu;

huifanya miguu yangu kama miguu ya ayala,

huniwezesha kupita juu ya vilima.

Kwa kiongozi wa uimbaji. Kwa vinanda vyangu vya nyuzi.

Source notes (1)
  1. Footnote Ni kifaa cha uimbaji chenye nyuzi; pia maombi kutumia kifaa hiki.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.