Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Habakuki 1

Neno la unabii alilopokea nabii Habakuki.

Lalamiko la Habakuki

Ee Mwenyezi Mungu, hata lini nitakuomba msaada,

lakini wewe husikilizi?

Au kukulilia, “Udhalimu!”

lakini hutaki kuokoa?

Kwa nini unanifanya nitazame dhuluma?

Kwa nini unavumilia makosa?

Uharibifu na udhalimu viko mbele yangu;

kuna mabishano na mapambano kwa wingi.

Kwa hiyo sheria imepotoshwa,

nayo haki haipo kabisa.

Waovu wanawazunguka wenye haki,

kwa hiyo haki imepotoshwa.

Jibu la Mwenyezi Mungu

“Yatazame mataifa,

uangalie na ushangae kabisa.

Kwa sababu katika siku zako nitafanya kitu

ambacho hungeamini,

hata kama ungeambiwa.

Tazama! Nitawainua Wakaldayo,

watu wakatili na wenye haraka,

ambao hupita dunia yote

ili kuteka makazi yasiyo yao.

Ni watu wanoogopwa na wanaotisha;

wenyewe ndio sheria yao,

na huinua heshima yao wenyewe.

Farasi wao ni wepesi kuliko chui,

na wakali kuliko mbwa-mwitu wakati wa machweo.

Askari wapanda farasi wao huenda mbio;

waendesha farasi wao wanatoka mbali.

Wanaruka kasi kama tai

ili kurarua mawindo;

wote wanakuja tayari kutenda udhalimu.

Makundi yao wanasonga mbele

kama upepo wa jangwani,

na kukusanya wafungwa

kama mchanga.

Wanawabeza wafalme,

na kuwadhihaki watawala.

Wanaicheka miji yote yenye ngome;

wanalundika udongo na kuiteka hiyo miji.

Kisha wanapita kasi kama upepo na kusonga mbele:

watu wenye hatia, ambao nguvu zao ndio mungu wao.”

Lalamiko la pili la Habakuki

Ee Mwenyezi Mungu, je, wewe sio wa tangu milele?

Mungu wangu, Uliye Mtakatifu wangu, hatutakufa.

Ee Mwenyezi Mungu, umewachagua wao ili watekeleze hukumu;

Ee Mwamba, umewaamuru watuadhibu.

Macho yako ni safi mno hata yasiweze kuutazama uovu,

wala huwezi kuvumilia makosa.

Kwa nini basi unawavumilia wadanganyifu?

Kwa nini unakuwa kimya wakati waovu

wanawameza wale wenye haki

kuliko wao wenyewe?

Umewafanya watu kama samaki baharini,

kama viumbe wa bahari wasio na mtawala.

Adui mwovu anawavuta wote kwa ndoana,

anawakamata katika wavu wake,

anawakusanya katika juya lake;

kwa hiyo anashangilia na anafurahi.

Kwa hiyo anatoa sadaka kwa wavu wake,

na kuchoma uvumba kwa juya lake,

kwa kuwa kwa wavu wake anaishi kwa starehe,

na anafurahia chakula kizuri.

Je, aendelee kuwatoa walio katika wavu wake,

akiangamiza mataifa bila huruma?

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.