Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Ezekieli 27

Maombolezo kwa ajili ya Tiro

Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: “Mwanadamu, fanya maombolezo kwa ajili ya Tiro. Umwambie Tiro, ulioko kwenye lango la bahari, ufanyao biashara na mataifa mengi ya pwani, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi:

“ ‘Ee Tiro, wewe umesema,

“Mimi ni mkamilifu katika uzuri.”

Mipaka yako ilikuwa katika moyo wa bahari,

wajenzi wako walikamilisha uzuri wako.

Walizifanya mbao zako zote

kwa misunobari kutoka Seniri1;

walichukua mwerezi kutoka Lebanoni

kukutengenezea mlingoti.

Walichukua mialoni kutoka Bashani

wakakutengenezea makasia yako;

kwa miti ya msanduku

kutoka pwani ya Kitimu

wakatengeneza sitaha yako

na kuipamba kwa pembe za ndovu.

Kitani safi kilichotariziwa kutoka Misri kilikuwa tanga lako,

nacho kilikuwa bendera yako;

chandarua chako kilikuwa cha rangi ya buluu na ya zambarau

kutoka visiwa vya Al-Yasa.

Wakaaji wa Sidoni na Arvadi walikuwa wapiga makasia yako;

watu wako wenye ustadi, ee Tiro,

ndio walikuwa mabaharia wako.

Wazee wa Gebali2 pamoja na mafundi stadi

walikuwa mafundi wako kwenye meli.

Meli zote za baharini na mabaharia wao

walikuja kwako ili kubadilishana bidhaa zako.

“ ‘Wanaume wa Uajemi, Ludi na Putu

walikuwa askari katika jeshi lako.

Walitundika ngao zao na chapeo zao kwenye kuta zako,

wakileta fahari yako.

Watu wa Arvadi na wa Heleki

walikuwa juu ya kuta zako pande zote;

watu wa Gamadi

walikuwa kwenye minara yako.

Walitundika ngao zao kuzizunguka kuta zako;

wakaukamilisha uzuri wako.

“ ‘Tarshishi walifanya biashara nawe kwa sababu ya utajiri wako mkubwa wa bidhaa, walibadilisha fedha, chuma, bati na risasi kwa mali yako.

“ ‘Uyunani, Tubali na Mesheki walifanya biashara nawe; walibadilisha binadamu na vyombo vya shaba kwa bidhaa zako.

“ ‘Watu wa Beth-Togarma walibadilisha farasi wa mizigo, farasi wa vita na nyumbu kwa mali yako.

“ ‘Watu wa Dedani3 walifanya biashara nawe, watu wengi wa nchi za pwani walikuwa wachuuzi wako, walikulipa kwa pembe za ndovu na mpingo.

“ ‘Watu wa Aramu walifanya biashara nawe kwa ajili ya wingi wa kazi za mikono yako, wakibadilishana kwa almasi, vitambaa vya rangi ya zambarau, vitambaa vilivyotariziwa, kitani safi, matumbawe4 na akiki nyekundu.

“ ‘Yuda na Israeli walifanya biashara nawe; walibadilishana ngano iliyotoka Minithi, mtama, asali, mafuta na zeri kwa bidhaa zako.

“ ‘Dameski walifanya biashara nawe kwa sababu ya wingi wa bidhaa zako na ukuu wa utajiri wa mali zako, wakibadilishana mvinyo kutoka Helboni na sufu kutoka Zahari.

“ ‘Wadani na Wayunani kutoka Uzali walikuletea mali ya biashara, nao wakabadilishana nawe chuma kilichofuliwa, mdalasini na mchaichai.

“ ‘Dedani alifanya biashara nawe kwa matandiko ya farasi.

“ ‘Arabuni na wakuu wote wa Kedari walikuwa wanunuzi wako; walifanya biashara nawe ya kubadilishana wana-kondoo, kondoo dume na mbuzi.

“ ‘Wafanyabiashara wa Sheba na wa Raama walifanya biashara nawe, wakabadilishana bidhaa zako na aina zote za vikolezo, vito vya thamani na dhahabu.

“ ‘Harani, Kane na Edeni na wafanyabiashara wa Sheba, Ashuru na Kilmadi walifanya biashara nawe. Kwenye soko lako, walifanya biashara nawe kwa mavazi mazuri, vitambaa vya buluu, nguo za kutariziwa na mazulia ya rangi mbalimbali yenye kamba zilizosokotwa na kuwekwa mafundo imara.

“ ‘Merikebu za Tarshishi ndizo

zinazokusafirishia bidhaa zako.

Umejazwa shehena kubwa

katika moyo wa bahari.

Wapiga makasia wako wanakupeleka

mpaka kwenye maji makuu.

Lakini upepo wa mashariki utakuvunja vipande vipande

moyoni mwa bahari.

Utajiri wako, bidhaa zako na mali yako,

mabaharia wako, manahodha wako,

mafundi wako wa meli,

wafanyabiashara wako na askari wako wote,

na kila mmoja aliye kwenye meli

atazama kwenye moyo wa bahari

siku ile meli yako itakapovunjika.

Nchi za pwani zitatetemeka

wakati mabaharia wako watakapopiga kelele.

Wote wapigao makasia

wataacha meli zao,

mabaharia wote na wanamaji wote

watasimama pwani.

Watapaza sauti zao

na kulia sana kwa ajili yako;

watajitupia mavumbi juu ya vichwa vyao

na kujivingirisha kwenye majivu.

Watanyoa nywele zao kwa ajili yako,

nao watavaa magunia.

Watakulilia kwa uchungu wa moyo

na kwa maombolezo makuu.

Watakapokuwa wanalia na kuomboleza juu yako,

watafanya maombolezo kukuhusu wakisema:

“Ni nani aliyepata kuangamizwa kama Tiro,

katika moyo wa bahari?”

Bidhaa zako zilipotoka baharini,

ulitosheleza mataifa mengi;

kwa wingi wa utajiri wako na bidhaa zako

ulitajirisha wafalme wa dunia.

Sasa umevunjavunjwa na bahari,

katika vilindi vya maji,

bidhaa zako na kundi lako lote

vimezama pamoja nawe.

Wote wanaoishi katika nchi za pwani

wanakustaajabia;

wafalme wao wanatetemeka kwa hofu kuu,

nazo nyuso zao zimekunjamana kwa woga.

Wafanyabiashara miongoni mwa mataifa wanakucheka;

umefikia mwisho wa kutisha

nawe hutakuwepo tena.’ ”

Source notes (4)
  1. Footnote yaani Mlima Hermoni
  2. Footnote yaani Bubilo
  3. Footnote yaani Rodo
  4. Footnote yaani marijani , jiwe la pwani au baharini

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.