Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Kutoka 30

Madhabahu ya kufukizia uvumba

(Kutoka 37:25-28)

“Tengeneza madhabahu kwa mbao za mshita kwa ajili ya kufukizia uvumba. Madhabahu hayo yawe mraba, urefu na upana wake dhiraa moja1, na kimo cha dhiraa mbili2, nazo pembe zake zitakuwa kitu kimoja nayo. Funika hayo madhabahu juu na pande zote na pia pembe zake kwa dhahabu safi, na uifanyizie ukingo wa dhahabu kuizunguka. Tengeneza pete mbili za dhahabu kwa ajili ya madhabahu chini ya huo ukingo, ziwe mbili kila upande, za kushikilia hiyo mipiko itumikayo kuibebea madhabahu. Tengeneza mipiko kwa miti ya mshita na uifunike kwa dhahabu. Weka hayo madhabahu mbele ya lile pazia lililo mbele ya Sanduku la ule Ushuhuda, lililo mbele ya kiti cha rehema kilicho juu ya ule Ushuhuda, mahali nitakapokutana nawe.

“Itampasa Haruni kufukiza uvumba wenye harufu nzuri juu ya madhabahu kila siku asubuhi wakati anapowasha zile taa. Itampasa afukize uvumba tena wakati anapowasha taa wakati wa machweo ili uvumba ufukizwe daima mbele za Mwenyezi Mungu kwa vizazi vijavyo. Usifukize uvumba mwingine wowote juu ya madhabahu haya au sadaka nyingine yoyote ya kuteketezwa wala sadaka ya nafaka, wala usimimine sadaka ya kinywaji juu yake. Mara moja kwa mwaka Haruni atafanya upatanisho juu ya pembe za hayo madhabahu. Upatanisho huu wa mwaka lazima ufanywe kwa damu ya sadaka ya upatanisho kwa ajili ya dhambi kwa vizazi vijavyo. Ni takatifu sana kwa Mwenyezi Mungu.”

Fedha ya upatanisho

Naye Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Utakapowahesabu Waisraeli, kila mmoja lazima alipe kwa Mwenyezi Mungu fidia kwa ajili ya nafsi yake wakati wa kuhesabiwa kwake. Ndipo hakutakuwa na pigo juu yao unapowahesabu. Kila mmoja anayeenda upande wa wale waliokwisha hesabiwa atatoa nusu shekeli3, kulingana na shekeli ya mahali patakatifu, ambayo ina uzito wa gera ishirini4. Hii nusu shekeli ni sadaka kwa Mwenyezi Mungu. Wote wanaovuka, wenye umri wa miaka ishirini au zaidi, watatoa sadaka kwa Mwenyezi Mungu. Matajiri hawatalipa zaidi ya nusu shekeli, nao maskini hawatatoa pungufu wakati mnatoa sadaka kwa Mwenyezi Mungu kwa kufanya upatanisho wa nafsi zenu. Utapokea fedha ya upatanisho kutoka kwa Waisraeli na uzitumie kwa ajili ya huduma ya Hema la Kukutania. Itakuwa ni ukumbusho kwa Waisraeli mbele za Mwenyezi Mungu kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu.”

Sinia la kunawia

Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Tengeneza sinia la shaba lenye kitako cha shaba kwa ajili ya kunawia. Liweke kati ya Hema la Kukutania na madhabahu, kisha uweke maji ndani yake. Haruni na wanawe watanawa mikono na miguu yao kwa maji ya hilo sinia. Wakati wowote wanapoingia katika Hema la Kukutania, watanawa kwa maji ili wasije wakafa. Pia, wanapokaribia madhabahu ili kuhudumu kwa kuleta sadaka zilizotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto, watanawa mikono na miguu yao ili wasije wakafa. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa Haruni na wazao wake kwa vizazi vijavyo.”

Mafuta ya upako

Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Chukua vikolezo bora vifuatavyo: shekeli mia tano5 za manemane ya maji, shekeli mia mbili na hamsini6 za mdalasini wenye harufu nzuri, shekeli mia mbili na hamsini za miwa yenye harufu nzuri, shekeli mia tano za aina nyingine ya mdalasini, vyote kulingana na shekeli ya mahali patakatifu, pia hini7 ya mafuta ya zeituni. Vitengeneze vikolezo hivi kuwa mafuta matakatifu ya upako yenye harufu nzuri, kazi ya mtengeneza manukato. Yatakuwa mafuta matakatifu ya upako. Kisha yatumie kupaka hilo Hema la Kukutania, Sanduku la Ushuhuda, meza na vifaa vyake vyote, kinara cha taa na vifaa vyake vyote, madhabahu ya kufukizia uvumba, madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na vyombo vyake vyote na sinia pamoja na kitako chake. Utaviweka wakfu ili viwe vitakatifu sana na kila kitakachoigusa kitakuwa kitakatifu.

“Mpake Haruni na wanawe mafuta na uwaweke wakfu ili waweze kunitumikia katika kazi ya ukuhani. Waambie Waisraeli, ‘Haya yatakuwa mafuta matakatifu yangu ya upako kwa vizazi vijavyo. Usiyamimine juu ya miili ya wanadamu wala usitengeneze mafuta ya aina nyingine kwa utaratibu huu. Ni mafuta matakatifu na ni lazima myaone kuwa ni matakatifu. Mtu yeyote atakayetengeneza manukato kama hayo na kuyamimina juu ya mtu ambaye si kuhani atakatiliwa mbali na watu wake.’ ”

Uvumba

Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Chukua vikolezo vyenye harufu nzuri vifuatavyo: natafi, shekelethi, kelbena na uvumba safi vyote vikiwa na vipimo sawa, pia tengeneza mchanganyiko wa uvumba wenye harufu nzuri, kazi ya mtengeneza manukato. Utiwe chumvi ili upate kuwa safi na mtakatifu. Saga baadhi yake kuwa unga na uweke mbele ya Sanduku la Ushuhuda ndani ya Hema la Kukutania, mahali nitakapokutana nawe. Itakuwa takatifu sana kwenu. Msitengeneze uvumba mwingine wowote wa namna hii kwa ajili yenu wenyewe; uoneni kuwa ni mtakatifu kwa Mwenyezi Mungu. Yeyote atakayetengeneza uvumba kama huu ili kufurahia harufu yake nzuri lazima akatiliwe mbali na watu wake.”

Source notes (7)
  1. Footnote Dhiraa moja ni sawa na sentimita 45.
  2. Footnote Dhiraa mbili ni sawa na sentimita 90.
  3. Footnote Nusu shekeli ni sawa na gramu 6.
  4. Footnote Gera 20 ni sawa na shekeli moja au gramu 12.
  5. Footnote Shekeli 500 ni sawa na kilo 6.
  6. Footnote Shekeli 250 ni sawa na kilo 3.
  7. Footnote Hini moja ni sawa na lita 4.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.