Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

2 Timotheo 3

Hatari za siku za mwisho

Lakini yakupasa ufahamu jambo hili: kwamba siku za mwisho kutakuwa na nyakati za hatari. Kwa maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kumkufuru Mungu, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio watakatifu, wasio na upendo, wasiopenda kupatanishwa, wasingiziaji, wasiozuia tamaa zao, wakatili, wasiopenda mema, wasaliti, wakaidi, waliojaa majivuno, wanaopenda anasa kuliko kumpenda Mungu: wakiwa na mfano wa utauwa kwa nje, lakini wakizikana nguvu za Mungu. Jiepushe na watu kama hao.

Miongoni mwao wamo wale wajiingizao katika nyumba za watu na kuwachukua mateka wanawake wajinga, waliolemewa na dhambi zao na kuyumbishwa na aina zote za tamaa mbaya. Hawa hujifunza siku zote, lakini kamwe hawawezi kuufikia ujuzi wa kweli. Kama vile Yane na Yambre walivyopingana na Musa, vivyo hivyo watu hawa hupingana na kweli. Hawa ni watu wenye akili zilizopotoka, ambao wamekataliwa kwa mambo ya imani. Lakini hawataendelea sana, kwa sababu upumbavu wao utakuwa dhahiri kwa watu wote, kama vile upumbavu wa hao watu wawili ulivyokuwa dhahiri.

Paulo amwagiza Timotheo

Lakini wewe umeyajua mafundisho yangu, mwenendo, makusudi, imani, uvumilivu, upendo, ustahimilivu, mateso na taabu, yaani mambo yote yaliyonipata huko Antiokia, Ikonio na Listra, mateso yote niliyostahimili, lakini Bwana Isa aliniokoa katika hayo yote. Naam, yeyote anayetaka kuishi maisha ya utauwa ndani ya Al-Masihi Isa atateswa. Lakini watu waovu na wadanganyaji watazidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika. Bali wewe, udumu katika yale uliyojifunza na kuyaamini kwa uthabiti, ukitambua ya kuwa ulijifunza hayo kutoka kwa nani, na jinsi tangu utoto umeyajua Maandiko Matakatifu, ambayo yanaweza kukuhekimisha upate wokovu kupitia kwa imani katika Al-Masihi Isa. Maandiko yote yamevuviwa na Mungu, na yafaa kwa mafundisho, kwa kuwaonya watu makosa yao, kwa kuwaongoza na kwa kuwafundisha katika haki, ili mtu wa Mungu awe amekamilishwa, apate kutenda kila kazi njema.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.