Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

2 Wathesalonike 1

Salamu

Paulo, Silvano1 na Timotheo.

Kwa kundi la waumini la Wathesalonike mlio katika Mungu, Baba2 yetu, na Bwana Isa Al-Masihi.

Neema na amani zinazotoka kwa Mungu Baba Mwenyezi na kwa Bwana Isa Al-Masihi ziwe nanyi.

Shukrani na maombi

Ndugu, inatupasa kumshukuru Mungu kwa ajili yenu siku zote, na inastahili hivyo kwa sababu imani yenu inazidi kukua sana, nao upendo wa kila mmoja wenu kwa mwenzake unazidi kuongezeka. Ndiyo sababu miongoni mwa makundi ya waumini ya Mungu, tunajivunia saburi yenu na imani mliyo nayo katika mateso yote na dhiki mnazostahimili.

Haya yote ni uthibitisho kwamba hukumu ya Mungu ni ya haki, na kwa sababu hiyo ninyi mtahesabiwa kwamba mnastahili kuwa wa ufalme wa Mungu, mnaoteswa kwa ajili yake. Mungu ni mwenye haki: yeye atawalipa mateso wale wanaowatesa ninyi, na kuwapa ninyi mnaoteseka amani pamoja na sisi, wakati Bwana Isa atadhihirishwa kutoka mbinguni katika mwali wa moto pamoja na malaika wake wenye nguvu. Atawaadhibu wale wasiomjua Mungu na ambao hawakuitii Injili ya Bwana wetu Isa. Wataadhibiwa kwa uangamivu wa milele na kutengwa na uso wa Mwenyezi Mungu na utukufu wa uweza wake, siku hiyo atakapokuja kutukuzwa katika watakatifu wake na kustaajabiwa miongoni mwa wote walioamini. Ninyi pia mtakuwa miongoni mwa hawa kwa sababu mliamini ushuhuda wetu kwenu.

Kwa sababu hii, tunawaombea ninyi bila kukoma, ili Mungu wetu apate kuwahesabu kuwa mnastahili wito wake na kwamba kwa uwezo wake apate kutimiza kila kusudi lenu jema na kila tendo linaloongozwa na imani yenu. Tunaomba hivi ili Jina la Bwana wetu Isa lipate kutukuzwa ndani yenu, nanyi ndani yake, kulingana na neema ya Mungu wetu na Bwana Isa Al-Masihi.

Source notes (2)
  1. Footnote yaani Sila
  2. Footnote Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.