Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

2 Nyakati 3

Sulemani ajenga Hekalu

(1 Wafalme 6:1-38; 7:15-22)

Ndipo Sulemani akaanza kujenga Hekalu la Mwenyezi Mungu katika Yerusalemu juu ya Mlima Moria, pale ambapo Mwenyezi Mungu alikuwa amemtokea Daudi baba yake. Ilikuwa katika kiwanja cha kupuria cha Arauna1 Myebusi, mahali palipotolewa na Daudi. Alianza kujenga siku ya pili ya mwezi wa pili katika mwaka wa nne wa utawala wake.

Msingi aliouweka Sulemani kwa ajili ya kulijenga Hekalu la Mungu ulikuwa na urefu wa dhiraa sitini2, na upana wa dhiraa ishirini3 kwa kipimo cha kale. Ukumbi wa mbele wa Hekalu ulikuwa na urefu wa dhiraa ishirini, yaani kuanzia upande mmoja hadi upande mwingine wa upana wa nyumba hiyo, na kimo chake dhiraa thelathini4.

Akaufunika ndani kwa dhahabu safi. Akaufunika ukumbi mkuu kwa mbao za msunobari, na kufunikwa kwa dhahabu safi, na kuupamba kwa michoro ya mitende na minyororo. Alilipamba Hekalu kwa vito vya thamani. Hiyo dhahabu aliyotumia ilikuwa dhahabu ya Parvaimu. Akazifunika boriti za dari, miimo na vizingiti vya milango, kuta na milango ya Hekalu kwa dhahabu, naye akatia nakshi ya makerubi kwenye kuta.

Akajenga Patakatifu pa Patakatifu, urefu na upana wake ulikuwa dhiraa ishirini, sawasawa na upana wa Hekalu. Alifunika ndani kwa talanta 6005 za dhahabu safi. Misumari ya dhahabu ilikuwa na uzito wa shekeli hamsini6. Alivifunika pia vyumba vya juu kwa dhahabu.

Katika sehemu ya Patakatifu pa Patakatifu akatengeneza jozi moja ya makerubi ya kuchongwa na kuyafunika kwa dhahabu. Urefu wa mabawa ya hao makerubi ulikuwa jumla ya dhiraa ishirini. Bawa moja la kerubi wa kwanza lilikuwa na urefu wa dhiraa tano7, nalo liligusa ukuta wa Hekalu; bawa lake lingine lilikuwa pia na urefu wa dhiraa tano, ambalo liligusa bawa la kerubi mwingine. Vivyo hivyo bawa moja la kerubi wa pili lilikuwa na urefu wa dhiraa tano na liligusa ukuta mwingine wa pili wa Hekalu, na bawa lake lingine lilikuwa pia na urefu wa dhiraa tano nalo liligusa bawa la kerubi wa kwanza. Mabawa ya makerubi hawa yalitanda dhiraa ishirini. Walisimama kwa miguu yao, nyuso zao zikielekea ukumbi mkubwa.

Akatengeneza pazia la nyuzi za rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na za kitani safi, na kutarizi makerubi juu yake.

Mbele ya Hekalu Sulemani akatengeneza nguzo mbili, ambazo kwa pamoja zilikuwa na urefu wa dhiraa thelathini na tano kwenda juu, na kila moja ilikuwa na taji juu yake yenye kimo cha dhiraa tano. Akatengeneza minyororo iliyosokotwa, na kuiweka juu ya zile nguzo. Pia akatengeneza makomamanga mia moja, na kuyaunganisha kwenye minyororo. Akazisimamisha hizo nguzo mbele ya Hekalu, moja upande wa kusini na nyingine upande wa kaskazini. Ile moja ya upande wa kusini akaiita Yakini8, na ya upande wa kaskazini akaiita Boazi9.

Source notes (9)
  1. Footnote au Ornani kwa Kiebrania
  2. Footnote Dhiraa 60 ni sawa na mita 27.
  3. Footnote Dhiraa 20 ni sawa na mita 9.
  4. Footnote Dhiraa 30 ni sawa na mita 13.5.
  5. Footnote Talanta 600 ni sawa na tani 21.
  6. Footnote Shekeli 50 ni sawa na gramu 600.
  7. Footnote Dhiraa 5 ni sawa na mita 2.25.
  8. Footnote maana yake Atathibitisha
  9. Footnote maana yake Imo nguvu

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.