Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
2 Nyakati 27
Yothamu mfalme wa Yuda
(2 Wafalme 15:32-38)
Yothamu alikuwa na umri wa miaka ishirini na tano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na sita. Mama yake aliitwa Yerusha binti Sadoki. Akafanya yaliyo mema machoni pa Mwenyezi Mungu kama Uzia baba yake alivyokuwa amefanya, lakini tofauti na yeye, hakuingilia huduma za hekaluni mwa Mwenyezi Mungu. Lakini hata hivyo, watu wakaendelea na desturi zao mbaya. Yothamu akajenga upya Lango la Juu la Hekalu la Mwenyezi Mungu na kufanya kazi kubwa kwenye ukuta katika kilima cha Ofeli. Akajenga miji katika nchi ya vilima ya Yuda, pamoja na ngome na minara mwituni.
Yothamu akafanya vita na mfalme wa Waamoni na kumshinda. Mwaka ule Waamoni wakamlipa talanta mia moja1 za fedha, kori elfu kumi2 za ngano, na kori elfu kumi za shayiri. Waamoni wakamletea kiasi hicho hicho mwaka wa pili na wa tatu.
Yothamu akaendelea kuwa na nguvu kwa sababu alienenda kwa ukamilifu mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wake.
Matukio mengine ya utawala wa Yothamu, pamoja na vita vyake vyote na vitu vingine alivyofanya, vimeandikwa katika kitabu cha wafalme wa Israeli na Yuda. Alikuwa na umri wa miaka ishirini na tano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na sita. Yothamu akalala na baba zake na akazikwa katika Mji wa Daudi. Naye Ahazi mwanawe akawa mfalme baada yake.
Source notes (2)
- Footnote Talanta 100 za fedha ni sawa na tani 3.75.
- Footnote Kori 10,000 za ngano ni sawa na tani 2.2.
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.
Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.