Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

1 Wafalme 4

Maafisa na watawala wa Sulemani

Basi Mfalme Sulemani akatawala Israeli yote.

Hawa walikuwa maafisa wake wakuu:

Kuhani: Azaria mwana wa Sadoki;

Elihorefu na Ahiya, wana wa Shisha: waandishi;

Yehoshafati mwana wa Ahiludi: karani;

Benaya mwana wa Yehoyada: jemadari mkuu wa jeshi;

Sadoki na Abiathari: makuhani;

Azaria mwana wa Nathani: kiongozi wa maafisa wa wilaya;

Zabudi mwana wa Nathani: kuhani na mshauri binafsi wa mfalme;

Ahishari: msimamizi wa jumba la kifalme;

Adoniramu mwana wa Abda: msimamizi wa kazi za kulazimisha.

Pia Sulemani alikuwa na watawala kumi na wawili wa wilaya katika Israeli yote, walioshughulikia mahitaji ya mfalme na ya watu wa nyumbani kwa mfalme. Kila mmoja alitoa chakula kwa mwezi mmoja katika mwaka.

Majina yao ni haya:

Ben-Huri: katika nchi ya vilima ya Efraimu;

Ben-Dekari: katika Makasi, Shaalbimu, Beth-Shemeshi na Elon-Beth-Hanani;

Ben-Hesedi: katika Arubothi (Soko na nchi yote ya Heferi zilikuwa zake);

Ben-Abinadabu: katika Nafoth-Dori (alimwoa Tafathi binti Sulemani);

Baana mwana wa Ahiludi: katika Taanaki na Megido, na katika Beth-Shani yote karibu na Sarethani chini ya Yezreeli, kuanzia Beth-Shani hadi Abel-Mehola kupita hadi Yokmeamu;

Ben-Geberi: katika Ramoth-Gileadi (makazi ya Yairi mwana wa Manase katika Gileadi ilikuwa yake, kadhalika wilaya ya Argobu katika Bashani na miji yake mikubwa sitini iliyozungukwa na kuta zenye makomeo ya shaba);

Ahinadabu mwana wa Ido: katika Mahanaimu;

Ahimaasi: katika Naftali (alikuwa amemwoa Basemathi binti Sulemani);

Baana mwana wa Hushai: katika Asheri na katika Bealothi;

Yehoshafati mwana wa Parua: katika Isakari;

Shimei mwana wa Ela: katika Benyamini;

Geberi mwana wa Uri: katika Gileadi (nchi ya Sihoni mfalme wa Waamori na nchi ya Ogu mfalme wa Bashani). Naye alikuwa mtawala pekee katika eneo hilo.

Mahitaji ya Sulemani ya kila siku

Watu wa Yuda na Israeli walikuwa wengi kama mchanga wa pwani; walikula, wakanywa na kufurahi. Mfalme Sulemani akatawala katika falme zote kuanzia Mto1 hadi nchi ya Wafilisti, hadi kwenye mpaka wa Misri. Nchi hizi zilileta ushuru na zilikuwa chini ya Sulemani, siku zote za maisha yake.

Mahitaji ya Sulemani ya kila siku yalikuwa kori thelathini2 za unga laini, kori sitini3 za unga wa kawaida. Ng’ombe kumi wa zizini, ng’ombe ishirini wa malisho, kondoo na mbuzi mia moja, pamoja na ayala, paa, kulungu na kuku wazuri sana. Kwa kuwa Sulemani alitawala falme zote magharibi ya Mto, kuanzia Tifsa hadi Gaza, naye akawa na amani pande zote. Wakati wa maisha ya Sulemani, watu wa Yuda na Israeli, kuanzia Dani hadi Beer-Sheba, waliishi salama, kila mtu chini ya mzabibu wake na chini ya mtini wake.

Sulemani alikuwa na mabanda elfu nne4 ya magari ya vita, na farasi elfu kumi na mbili.

Maafisa wa eneo hilo, kila mmoja katika mwezi wake, walileta mahitaji kwa ajili ya Mfalme Sulemani na wote waliokula mezani mwa mfalme. Walihakikisha kuwa hakuna chochote kilichopungua. Pia walileta kiasi walichopangiwa cha shayiri na majani kwa ajili ya farasi wa magari ya vita na farasi wengine mahali palipostahili.

Hekima ya Sulemani

Mungu akampa Sulemani hekima na akili kubwa, pia ufahamu mpana usiopimika kama mchanga ulioko pwani ya bahari. Hekima ya Sulemani ilikuwa kubwa kuliko hekima ya watu wote wa Mashariki na kubwa kuliko hekima yote ya Misri. Alikuwa na hekima kuliko kila mwandishi, akiwemo Ethani Mwezrahi; kuliko Hemani, Kalkoli na Darda, wana wa Maholi. Umaarufu wake ukaenea kwa mataifa yote yaliyomzunguka. Akanena mithali elfu tatu, na nyimbo zake zilikuwa elfu moja na tano (1,005). Akaelezea maisha ya mimea kuanzia mwerezi wa Lebanoni hadi hisopo iotayo ukutani. Pia akafundisha kuhusu wanyama na ndege, wanyama wanaotambaa na samaki. Watu wa mataifa yote wakaja kusikiliza hekima ya Sulemani, wakiwa wametumwa na wafalme wote wa ulimwengu, waliokuwa wamesikia kuhusu hekima yake.

Source notes (4)
  1. Footnote yaani Mto Frati
  2. Footnote Kori 30 ni sawa na madebe 360.
  3. Footnote Kori 60 ni sawa na madebe 720.
  4. Footnote maandishi mengine yanasema elfu arobaini (taz. 2 Nyakati 9:25 ).

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.