Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™

Zaburi 50

Ibada Ya Kweli

Zaburi ya Asafu.

Mwenye Nguvu, Mungu, Bwana,

asema na kuiita dunia,

tangu mawio ya jua

hadi mahali pake liendapo kutua.

Kutoka Sayuni, penye uzuri mkamilifu,

Mungu anaangaza.

Mungu wetu anakuja na hatakaa kimya,

moto uteketezao unamtangulia,

akiwa amezungukwa na tufani kali.

Anaziita mbingu zilizo juu,

na nchi, ili aweze kuwahukumu watu wake:

“Nikusanyieni watu wangu waliowekwa wakfu,

waliofanya agano nami kwa dhabihu.”

Nazo mbingu zinatangaza haki yake,

kwa maana Mungu mwenyewe ni hakimu.

“Sikieni, enyi watu wangu, nami nitasema,

ee Israeli, nami nitashuhudia dhidi yenu:

Mimi ndimi Mungu, Mungu wenu.

Sikukemei kwa sababu ya dhabihu zako,

au sadaka zako za kuteketezwa,

ambazo daima ziko mbele zangu.

Sina haja ya fahali wa banda lako,

au mbuzi wa zizi lako.

Kwa maana kila mnyama wa msituni ni wangu,

na pia makundi ya mifugo juu ya vilima elfu.

Ninamjua kila ndege mlimani,

nao viumbe wa kondeni ni wangu.

Kama ningekuwa na njaa, nisingewaambia ninyi,

kwa maana ulimwengu ni wangu,

pamoja na vyote vilivyomo ndani yake.

Je, mimi hula nyama ya mafahali

au kunywa damu ya mbuzi?

Toa sadaka za shukrani kwa Mungu,

timiza nadhiri zako kwake Yeye Aliye Juu Sana,

na uniite siku ya taabu;

nami nitakuokoa, nawe utanitukuza.”

Lakini kwake mtu mwovu, Mungu asema:

“Una haki gani kunena sheria zangu

au kuchukua agano langu midomoni mwako?

Unachukia mafundisho yangu

na kuyatupa maneno yangu nyuma yako.

Unapomwona mwizi, unaungana naye,

unapiga kura yako pamoja na wazinzi.

Unakitumia kinywa chako kwa mabaya

na kuuongoza ulimi wako kwa hila.

Wanena daima dhidi ya ndugu yako

na kumsingizia mwana wa mama yako.

Mambo haya unayafanya, nami nimekaa kimya,

ukafikiri Mimi nami ni kama wewe.

Lakini nitakukemea

na kuweka mashtaka mbele yako.

“Yatafakarini haya, ninyi mnaomsahau Mungu,

ama sivyo nitawararua vipande vipande,

wala hapatakuwepo na yeyote wa kuwaokoa:

Atoaye dhabihu za shukrani ananiheshimu mimi,

naye aiandaa njia yake

ili nimwonyeshe wokovu wa Mungu.”

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.