Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™

Zaburi 115

Mungu Mmoja Wa Kweli

Sio kwetu sisi, Ee Bwana, sio kwetu sisi,

bali utukufu ni kwa jina lako,

kwa sababu ya upendo

na uaminifu wako.

Kwa nini mataifa waseme,

“Yuko wapi Mungu wao?”

Mungu wetu yuko mbinguni,

naye hufanya lolote limpendezalo.

Lakini sanamu zao ni za fedha na dhahabu,

zilizotengenezwa kwa mikono ya wanadamu.

Zina vinywa, lakini haziwezi kusema,

zina macho, lakini haziwezi kuona;

zina masikio, lakini haziwezi kusikia,

zina pua, lakini haziwezi kunusa;

zina mikono, lakini haziwezi kupapasa,

zina miguu, lakini haziwezi kutembea;

wala koo zao haziwezi kutoa sauti.

Wale wanaozitengeneza watafanana nazo,

vivyo hivyo wale wote wanaozitumainia.

Ee nyumba ya Israeli, mtumainini Bwana,

yeye ni msaada na ngao yao.

Ee nyumba ya Aroni, mtumainini Bwana,

yeye ni msaada na ngao yao.

Ninyi mnaomcha, mtumainini Bwana,

yeye ni msaada na ngao yao.

Bwana anatukumbuka na atatubariki:

ataibariki nyumba ya Israeli,

ataibariki nyumba ya Aroni,

atawabariki wale wanaomcha Bwana,

wadogo kwa wakubwa.

Bwana na awawezeshe kuongezeka,

ninyi na watoto wenu.

Mbarikiwe na Bwana

Muumba wa mbingu na dunia.

Mbingu zilizo juu sana ni mali ya Bwana,

lakini dunia amempa mwanadamu.

Sio wafu wanaomsifu Bwana,

wale washukao mahali pa kimya,1

bali ni sisi tunaomtukuza Bwana,

sasa na hata milele.

Msifuni Bwana.2

Source notes (2)
  1. Footnote Mahali pa kimya maana yake ni Kuzimu, yaani Sheol kwa Kiebrania.
  2. Footnote Msifuni Bwana ni Kiebrania Hallelu Yah.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.