Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™
Zaburi 113
Kumsifu Bwana Kwa Wema Wake
Msifuni Bwana.
Enyi watumishi wa Bwana msifuni,
lisifuni jina la Bwana.
Jina la Bwana na lisifiwe,
sasa na hata milele.
Kuanzia mawio ya jua hadi machweo yake,
jina la Bwana linapaswa kusifiwa.
Bwana ametukuka juu ya mataifa yote,
utukufu wake juu ya mbingu.
Ni nani aliye kama Bwana Mungu wetu,
Yeye ambaye ameketi juu kwenye kiti cha enzi,
ambaye huinama atazame chini
aone mbingu na nchi?
Huwainua maskini kutoka mavumbini,
na kuwanyanyua wahitaji kutoka kwenye jalala,
huwaketisha pamoja na wakuu,
pamoja na wakuu wa watu wake.
Humjalia mwanamke tasa kutulia nyumbani mwake,
akiwa mama watoto mwenye furaha.
Msifuni Bwana.
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.
Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.