Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™

Yona 2

Maombi Ya Yona Katika Tumbo La Nyangumi

Akiwa ndani ya tumbo la nyangumi, Yona alimwomba Bwana Mungu wake. Akasema:

“Katika shida yangu nalimwita Bwana,

naye akanijibu.

Kutoka kina cha kaburi1 niliomba msaada,

nawe ukasikiliza kilio changu.

Ulinitupa kwenye kilindi,

ndani kabisa ya moyo wa bahari,

mikondo ya maji ilinizunguka,

mawimbi yako yote na viwimbi

vilipita juu yangu.

Nikasema, ‘Nimefukuziwa

mbali na uso wako,

hata hivyo nitatazama tena

kuelekea Hekalu lako takatifu.’

Maji yaliyonimeza yalinitisha,

kilindi kilinizunguka;

mwani2 ulijisokota kichwani pangu.

Nilizama chini sana mpaka pande za mwisho za milima,

makomeo ya hiyo nchi yalinifungia hata milele.

Lakini uliuleta uhai wangu kutoka shimoni,

Ee Bwana Mungu wangu.

“Wakati uhai wangu ulipokuwa unatoka,

nilikukumbuka wewe, Bwana,

nayo maombi yangu yalikufikia wewe,

katika Hekalu lako takatifu.

“Wale watu wanaongʼangʼana na sanamu zisizofaa

hupoteza neema ile ambayo ingekuwa yao.

Lakini mimi, kwa wimbo wa shukrani,

nitakutolea dhabihu.

Lile nililowekea nadhiri nitalitimiza.

Wokovu watoka kwa Bwana.”

Basi Bwana akamwamuru yule nyangumi, naye akamtapika Yona katika nchi kavu.

Source notes (2)
  1. Footnote Kaburi hapa maana yake ni Kuzimu, kwa Kiebrania ni Sheol.
  2. Footnote Mwani hapa maana yake ni magugu yaotayo kwenye sakafu ya kilindi cha bahari.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.