Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™

Ayubu 35

Elihu Analaumu Mtu Kujiona Kuwa Mwenye Haki

Ndipo Elihu akasema:

“Je, unadhani hili ni haki?

Wewe unasema, ‘Nina haki mbele za Mungu.’

Bado unamuuliza, ‘Ni faida gani nimepata,

na imenifaidi nini kwa kutokutenda dhambi?’

“Ningependa nikujibu wewe

pamoja na marafiki zako walio pamoja nawe.

Tazama juu mbinguni ukaone;

yaangalie mawingu yaliyo juu sana juu yako.

Je, ukitenda dhambi, inamdhuruje Mungu?

Kama dhambi zako zikiwa nyingi,

hilo linamfanyia nini Mungu?

Kama wewe ni mwadilifu, unampa nini,

au yeye anapokea nini mkononi kwako?

Uovu wako unamdhuru tu mtu mwingine kama wewe,

nayo haki yako inawafaa wanadamu tu.

“Wanadamu hulia kwa kulemewa na mateso;

huomba msaada kutoka mkono wenye nguvu.

Lakini hakuna asemaye, ‘Yuko wapi Mungu Muumba wangu,

yeye anifanyaye niimbe usiku,

yeye atufundishaye sisi zaidi kuliko wanyama wa dunia,

na kutufanya wenye hekima kuliko ndege wa angani?’

Yeye hajibu wakati watu waliapo

kwa sababu ya kiburi cha watu waovu.

Naam, Mungu hasikilizi maombi yao ya ubatili;

Mwenyezi hayazingatii.

Si zaidi sana kwamba hatakusikiliza

wewe usemapo humwoni,

tena ya kwamba shauri lako liko mbele zake

na wewe lazima umngojee,

pia zaidi, kwamba hasira yake kamwe haiadhibu

wala haangalii uovu hata kidogo?

Hivyo Ayubu hufumbua kinywa chake kwa maneno yasiyo na maana;

anaongea maneno mengi bila maarifa.”

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.