Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™

Yeremia 47

Ujumbe Kuhusu Wafilisti

Hili ndilo neno la Bwana lililomjia nabii Yeremia kuhusu Wafilisti, kabla Farao hajaishambulia Gaza:

Hili ndilo asemalo Bwana:

“Tazama jinsi maji yanavyoinuka huko kaskazini,

yatakuwa mafuriko yenye nguvu sana.

Yataifurikia nchi na vitu vyote vilivyomo ndani yake,

miji na wale waishio ndani yake.

Watu watapiga kelele;

wote waishio katika nchi wataomboleza

kwa sauti ya kwato za farasi waendao mbio,

kwa sauti ya magari ya adui

na mngurumo wa magurudumu yake.

Baba hawatageuka kuwasaidia watoto wao,

mikono yao italegea.

Kwa maana siku imewadia

kuwaangamiza Wafilisti wote

na kuwakatilia mbali walionusurika wote

ambao wangeweza kusaidia Tiro na Sidoni.

Bwana anakaribia kuwaangamiza Wafilisti,

mabaki toka pwani za Kaftori.1

Gaza atanyoa kichwa chake katika kuomboleza,

Ashkeloni atanyamazishwa.

Enyi mabaki kwenye tambarare,

mtajikatakata wenyewe mpaka lini?

“Mnalia, ‘Aa, upanga wa Bwana,

utaendelea mpaka lini ndipo upumzike?

Rudi ndani ya ala yako;

acha na utulie.’

Lakini upanga utatuliaje

wakati Bwana ameuamuru,

wakati ameuagiza kuishambulia Ashkeloni

pamoja na pwani yake?”

Source notes (1)
  1. Footnote Kaftori ndio Krete.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.