Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™

Isaya 62

Jina Jipya La Sayuni

Kwa ajili ya Sayuni sitanyamaza,

kwa ajili ya Yerusalemu sitatulia,

mpaka haki yake itakapoangaza kama mapambazuko,

wokovu wake kama mwanga wa moto.

Mataifa wataona haki yako,

nao wafalme wote wataona utukufu wako;

wewe utaitwa kwa jina jipya

lile ambalo kinywa cha Bwana kitatamka.

Utakuwa taji ya fahari mkononi mwa Bwana,

taji ya kifalme mkononi mwa Mungu wako.

Hawatakuita tena Aliyeachwa,

wala nchi yako kuiita Ukiwa.

Bali utaitwa Hefsiba,1

nayo nchi yako itaitwa Beula,2

kwa maana Bwana atakufurahia,

nayo nchi yako itaolewa.

Kama vile kijana aoavyo mwanamwali,

ndivyo wanao3 watakavyokuoa wewe;

kama bwana arusi amfurahiavyo bibi arusi wake,

ndivyo Mungu wako atakavyokufurahia wewe.

Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, ee Yerusalemu,

hawatanyamaza mchana wala usiku.

Ninyi wenye kumwita Bwana,

msitulie,

msimwache apumzike hadi atakapoufanya imara Yerusalemu

na kuufanya uwe sifa ya dunia.

Bwana ameapa kwa mkono wake wa kuume

na kwa mkono wake wenye nguvu:

“Kamwe sitawapa tena adui zenu

nafaka zenu kama chakula chao;

kamwe wageni hawatakunywa tena

divai mpya ambayo mmeitaabikia,

lakini wale waivunao nafaka wataila

na kumsifu Bwana,

nao wale wakusanyao zabibu watainywa divai yake

katika nyua za patakatifu pangu.”

Piteni, piteni katika malango!

Tengenezeni njia kwa ajili ya watu.

Jengeni, jengeni njia kuu!

Ondoeni mawe.

Inueni bendera kwa ajili ya mataifa.

Bwana ametoa tangazo

mpaka miisho ya dunia:

“Mwambie Binti Sayuni,

‘Tazama, mwokozi wako anakuja!

Tazama ujira wake uko pamoja naye,

na malipo yake yanafuatana naye!’ ”

Wataitwa Watu Watakatifu,

Waliokombolewa na Bwana;

nawe utaitwa Aliyetafutwa,

Mji Usioachwa Tena.

Source notes (3)
  1. Footnote Hefsiba maana yake Yeye ninayemfurahia.
  2. Footnote Beula maana yake Aliyeolewa.
  3. Footnote Au: wajenzi wako.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.