Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™

Hosea 4

Shtaka Dhidi Ya Israeli

Sikieni neno la Bwana, enyi Waisraeli,

kwa sababu Bwana analo shtaka

dhidi yenu ninyi mnaoishi katika nchi:

“Hakuna uaminifu, hakuna upendo,

hakuna kumjua Mungu katika nchi.

Kuna kulaani tu, uongo na uuaji,

wizi na uzinzi,

bila kuwa na mipaka,

nao umwagaji damu mmoja

baada ya mwingine.

Kwa sababu hii nchi huomboleza,

wote waishio ndani mwake wanadhoofika,

wanyama wa kondeni, ndege wa angani

na samaki wa baharini wanakufa.

“Lakini mtu awaye yote na asilete shtaka,

mtu yeyote na asimlaumu mwenzake,

kwa maana watu wako ni kama wale

waletao mashtaka dhidi ya kuhani.

Unajikwaa usiku na mchana,

nao manabii hujikwaa pamoja nawe.

Kwa hiyo nitamwangamiza mama yako:

watu wangu wanaangamizwa

kwa kukosa maarifa,

“Kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa,

mimi nami nitakukataa wewe

usiwe kuhani kwangu mimi;

kwa kuwa umeacha kuijali sheria ya Mungu wako

mimi nami sitawajali watoto wako.

Kadiri makuhani walivyoongezeka,

ndivyo walivyozidi kutenda dhambi dhidi yangu,

walibadilisha utukufu wao kwa kitu cha aibu.

Hujilisha dhambi za watu wangu

na kupendezwa na uovu wao.

Hata itakuwa: Kama walivyo watu,

ndivyo walivyo makuhani.

Nitawaadhibu wote wawili kwa ajili ya njia zao

na kuwalipa kwa matendo yao.

“Watakula lakini hawatashiba;

watajiingiza katika ukahaba

lakini hawataongezeka,

kwa sababu wamemwacha Bwana

na kujiingiza wenyewe

katika ukahaba,

divai ya zamani na divai mpya,

ambavyo huondoa ufahamu

wa watu wangu.

Hutaka shauri kutoka kwa sanamu ya mti

nao hujibiwa na fimbo ya mti.

Roho ya ukahaba imewapotosha,

hawana uaminifu kwa Mungu wao.

Wanatoa dhabihu juu ya vilele vya milima

na sadaka za kuteketezwa juu ya vilima,

chini ya mialoni, milibua na miela,

ambako kuna vivuli vizuri.

Kwa hiyo binti zenu wamegeukia ukahaba

na wake za wana wenu uzinzi.

“Sitawaadhibu binti zenu wakati

wanapogeukia ukahaba,

wala wake za wana wenu

wanapofanya uzinzi,

kwa sababu wanaume wenyewe huandamana na malaya

na kutambikia pamoja na makahaba

wa mahali pa kuabudia miungu:

watu wasiokuwa na ufahamu

wataangamia!

“Ingawa umefanya uzinzi, ee Israeli,

Yuda naye asije akawa na hatia.

“Usiende Gilgali,

usipande kwenda Beth-Aveni1

Wala usiape,

‘Hakika kama Bwana aishivyo!’

Waisraeli ni wakaidi,

kama mtamba wa ngʼombe ambaye ni mkaidi.

Ni jinsi gani basi Bwana anaweza kuwachunga

kama wana-kondoo

katika shamba la majani?

Efraimu amejiunga na sanamu,

ondokana naye!

Hata wakati wamemaliza vileo vyao

wanaendelea na ukahaba wao,

watawala wao hupenda sana

njia za aibu.

Kisulisuli kitawafagilia mbali

na dhabihu zao zitawaletea aibu.

Source notes (1)
  1. Footnote Beth-Aveni maana yake Nyumba ya Ubatili (au Uovu), jina lingine la Betheli kwa dhihaka.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.