Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™

Kumbukumbu 34

Kifo Cha Mose

Kisha Mose akaupanda mlima Nebo kutoka tambarare za Moabu mpaka kilele cha Pisga, ngʼambo ya Yeriko. Huko Bwana akamwonyesha nchi yote: kutoka Gileadi mpaka Dani, Naftali yote, nchi ya Efraimu na Manase, nchi yote ya Yuda mpaka bahari ya magharibi,1 Negebu na nchi yote kuanzia Bonde la Yeriko, Mji wa Mitende, hadi Soari. Kisha Bwana akamwambia, “Hii ndiyo nchi niliyomwahidi Abrahamu na Isaki na Yakobo kwa kiapo niliposema, ‘Nitawapa wazao wako.’ Nimekuruhusu uione kwa macho yako, lakini hutavuka kuingia.”

Naye Mose mtumishi wa Bwana akafa huko Moabu, kama Bwana alivyokuwa amesema. Mungu akamzika huko Moabu, katika bonde mkabala na Beth-Peori, lakini hakuna ajuaye kaburi lake lilipo mpaka leo. Mose alikuwa na umri wa miaka mia moja na ishirini alipofariki; hata hivyo nguvu ya macho yake haikufifia wala mwili wake haukudhoofika. Waisraeli wakaomboleza kwa ajili ya Mose kwenye tambarare za Moabu kwa siku thelathini, mpaka wakati wa kulia na kuomboleza ulipopita.

Basi Yoshua mwana wa Nuni alijazwa roho ya hekima kwa sababu Mose alikuwa ameweka mikono yake juu yake. Kwa hiyo Waisraeli wakamsikiliza na wakafanya yale ambayo Bwana alikuwa amemwagiza Mose.

Tangu wakati huo, katika Israeli hajainuka nabii mwingine kama Mose, ambaye Bwana alimjua uso kwa uso, aliyetenda ishara zote zile za miujiza na maajabu ambayo Bwana alimtuma kuyatenda huko Misri, yaani kwa Farao na maafisa wake wote na nchi yake yote. Kwa kuwa hakuna mtu yeyote aliyewahi kuonyesha nguvu nyingi ama kutenda matendo ya kutisha ambayo Mose aliwahi kuyafanya mbele ya Israeli yote.

Source notes (1)
  1. Footnote Yaani Bahari ya Mediterania.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.