Biblia Takatifu
Zaburi 142
Zaburi ya Daudi, alipokuwa pangoni; maombi.
Kwa sauti yangu namlilia Yahwe anisaidie; kwa sauti yangu naomba kwa ajili ya neema ya Yahwe. Namwaga malalamiko yangu mbele zake; ninamwambia shida zangu. Roho yangu inapokuwa dhaifu ndani yangu, wewe unajua mapito yangu. Kwenye njia niipitayo wamenifichia mtego. Natazama kulia kwangu na sioni yeyote anayenijali. Sina pa kukimbilia; hakuna anayejali kuhusu uhai wangu. Nilikuita wewe, Yahwe; nikasema, “Wewe ni kimbilio langu, fungu langu katika nchi ya walio hai. Sikia kuita kwangu, maana nimeshushwa chini sana; uniokoe dhidi ya watesi wangu, maana wana nguvu kuliko mimi. Uitoe nafsi yangu kifungoni ili niweze kulishukuru jina lako. Wenye haki watakusanyika karibu nami kwa sababu umekuwa mwema kwangu.”
Swahili Unlocked Literal Bible / Biblia Takatifu. Copyright © 2019 Door43 World Missions Community. Translation and contributors: see the complete source notice below. Licensed under CC BY-SA 4.0. Typeset from the source USFM; no intended changes to scripture wording.
Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.